Kwa ujumla, kikao hicho kilikuwa cha kuelimisha, kuvutia na chenye athari chanya, kikiwapa washiriki maarifa sahihi ya kitabibu pamoja na hamasa ya kuchukua hatua za kinga kwa ajili ya kulinda afya zao, familia zao na jamii kwa ujumla. Falah Islamic Development ilipongezwa kwa mchango wake katika kuhamasisha elimu ya afya na ustawi wa jamii.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt as -ABNA- Shirika la Falah Islamic Development limefanikiwa kuandaa na kuendesha kikao muhimu cha elimu ya afya kilichofanyika siku ya Alhamisi tarehe 18 Disemba 2025, kikijikita katika mada nyeti ya “Hepatitis B na Chanjo”, kwa lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu ugonjwa huo hatari na namna bora za kujikinga.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wanajamii mbalimbali na kiliongozwa na Dkt. Sadiq Dawood, ambaye aliwasilisha mada kwa njia iliyo wazi, ya kitaalamu na inayofahamika kwa urahisi. Katika maelezo yake, Dkt. Sadiq alifafanua kwa kina ugonjwa wa Hepatitis B, akieleza kuwa ni maambukizi ya virusi yanayoshambulia ini na yanaweza kusababisha madhara makubwa ya kiafya endapo hayatagunduliwa na kutibiwa mapema.

Aidha, alieleza njia kuu za maambukizi ya Hepatitis B, ikiwemo kuambukizwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua, matumizi ya vifaa vyenye ncha kali visivyo salama, pamoja na kuhusiana kwa karibu na mtu aliyeambukizwa. Alisisitiza pia hatari za muda mrefu za ugonjwa huo, kama vile kuharibika kwa ini, saratani ya ini, na matatizo sugu ya kiafya yanayoweza kuhatarisha maisha.

Katika sehemu muhimu ya mawasilisho yake, Dkt. Sadiq alihimiza umuhimu wa chanjo ya Hepatitis B kama njia salama na yenye ufanisi mkubwa wa kinga, akiwataka wazazi, vijana na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanapata chanjo kwa wakati unaostahili.

Your Comment